Waziri wa kazi nchini Msumbiji Helena Taipo amemfukuza nchini kocha wa klabu ya soka kwa kuwakashifu wananchi wa nchi hiyo.
Diamantino Miranda, ambae ni Mreno na kocha wa klabu ya Costa do Sol mjini Maputo, lazima aondoke nchini ifikapo Jumaamosi. .
Mnamo mwezi uliopita alinukiliwa akisema Wanamsumbiji ni "genge la wevi" baada ya kutokubaliana na uamuzi wa refa.
Ameomba radhi na kulia machozi alipokutana na waandishi habari kutangaza kwamba amefukuzwa nchini.
Kocha huyo alisema awali alipotamka maneno hayo kwa mwaandishi habari mmoja hakujua kua yalikuwa yanarekodiwa
Akizungumza kwa majonzi katika mkutano na waandishi habari ulioitishwa na Costa do Sol, mojawapo wa vilabu vikubwa nchini humo,alisema anawaheshimu sana wananchi wa Msumbiji na daima wako katika moyo wake.
"natumai ukweli utadhihiri na siku moja nitarejea Msumbiji " alinukiliwa na gazeti la Publico la Ureno"
Matamshi ya Miranda yalitolewa baada ya Costa do Sol kushindwa 2-1 na Vilanculos mwezi uliopita.
"wote hapa ni wevi .Nyote hapa ni genge la wevi.Wewe na waandishi wengine mnaweza kununuliwa kwa bakuli la supu tu. Nchi hii ni mzaha tu," alirekodiwa akisema.
Wakuu wa klabu ya Costa do Sol wamesema hawakubaliani na amri ya kumfukuza nchini na wanahisi si haki.
Barua ya kumfukuza nchini iliwasilishwa kwa klabu hiyo siku ya Alkhamisi na ikimaanisha Bw.Miranda alipewa saa 48 kuondoka nchini.
Barua ya waziri ilisema " alionyesha utovu wa heshima,ustaarabu na kupuuza maadili ya katiba ya Jamhuri na sheria za nchi yetu," kwa mujibu wa gazeti la O Pais la Msumbiji.
Takriban Wareno 250,000 waliondoka Msumbiji baada ya uhuru mwaka 1975 lakini wengi sasa wanatafuta ajira katika koloni hilo la zamani la Ureno ambako uchumi wake ni miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi sana duniani tofauti na ilivyo nchini Ureno.
No comments:
Post a Comment