Kocha wa zamani wa Manchester City ,Roberto Mancini anazungumza na mabingwa wa Uturuki Galatasaray kuhusu nafasi iliyo wazi ya kocha wa klabu hiyo.
Klabu hiyo ya mjini Istanbul ilithibitisha katika mtandao wa Twitter kwamba Mancini amekutana na wakurugenzi wa klabu hiyo na kupigwa picha na mkurugenzi mkuu , Lutfi Aribogan.
Mtaliana huyo anatarajiwa kushika nafasi ya Fatih Terim, ambae alipigwa kalamu wiki iliyopita baada ya kushindwa kukubaliana mkataba mpya.
Manchester City ilimfuta Mancini mnamo mwezi wa Mei mwaka mmoja baada ya kuongoza hadi kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya England.
Galatasaray imeanza vibaya msimu wa soka Uturuki ikishinda mechi moja tu kati ya michuano mitano ya kwanza .
Katika michuano ya klabu bingwa ya Ulaya ilicharazwa na Real Madrid,kwa mabao 6-1.
Terim, mwenye umri wa miaka 60, aliongoza Galatasary kushinda mara 6 ubingwa wa Uturuki pamoja na kombe la UEFA mwaka 2000 baada ya kuichezea kwa kipindi cha miaka 11.
Mancini ameshinda ubingwa wa Italia mara tatu akiwa na Inter Milan ya Utaliana kabla ya kunyakua kombe la FA na ubingwa wa ligi na Manchester City.
No comments:
Post a Comment